Adhabu ya mauaji ni kifo Somalia

Image caption Wanajeshi zaidi Somalia watapata hukumu sawa na hii kwa kutenda uhalifu bila kujali

Mwanajeshi mmoja nchini Somalia ameuawa kwa kupigwa risasi na kikundi cha wanjeshi na polisi mjini Mogadishu , baada ya mahakama ya kijeshi kuamuru kuuawa kwake.

Uamuzi wa mahakama ulitokana na madai kuwa mwanajeshi huyo alimuua mwanafunzi mwaka jana.

umati wa watu wakiwemo watoto walishuhudia kuuawa kwa mwanajeshi huyo, katika kituo cha mafunzo cha wanajeshi mjini Mogadishu kwa mujibu wa picha zilizowekwa kwenye mtandano wa kisomali wa redio Shabelle.

Hukumu ya mauaji nchini Somalia ni kifo.

Wanajeshi wa serikali mara kwa mara hutuhumiwa kwa kufanya vitendo vya uhalifu bila kujali ikiwemo mauaji na ubakaji.

Kituo cha Redio kiliripoti kuwa wanajeshi zaidi watakaopatikana na hatia ya mauaji huenda wakakabiliwa na adhabu sawa na hiyo katika siku zijazo.

Maslah Isse Jimaan alihukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa shule katika soko rasmi la Bakara, alipokuwa anashika doria mwaka jana.

Aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi pamoja na wanajeshi kumi walioonekana katika picha hiyo kabla ya Jimaan, kufumbwa macho na kufungwa kwenye mlingoti na kisha kupigwa risasi mbele ya umati wa watu.

'Jimaan alikuwa amekiuka kanuni za jeshi, na hii ndio ilikuwa adhabu yake,' alisema mwenyekiti wa mahakama ya kijeshi Libaan Ali Yarow.

Hata hivyo bwana Yarow alisema kuwa hakua na habari kuwa Jimmah aliuawa mbele ya watoto.