Karegeya: Uchunguzi kuharakishwa

Image caption Karegeya alikuwa mshirika wa karibu sana wa Rais Paul Kagame kabla ya kutofautiana

Serikali ya Afrika Kusini imeamrisha kuharakishwa kwa uchunguzi kuhusu mauaji nchini humo ya aliyekuwa mkuu wa ujasusi nchini Rwanda Patrick Karegeya.

Hadi sasa polisi wangali kumkamata hata mshukiwa mmoja kuhusiana na mauaji hayo siku tisa tangu kuuawa kwake.

Uchunguzi wa mapema unaonyesha kuwa kulikuwa na mvutano kati ya Karegeya na mtu aliyemuua kabla ya kifo chake. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya waziri wa sheria katika tamko la kwanza la serikali ya nchi hiyo tangu kutokea kifo cha Karegeya.

Mapema Alhamisi Chama cha upinzani cha Rwanda National Congress leo kiliandaa maandamano ya raia wa Rwanda wanaoishi Afrika Kusini hadi makao ya ubalozi wa taifa hilo mjini Pretoria kulalamikia mauaji ya aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi Kanali Patrick Karegeya .

Raia hao walikilaani walichoita mauaji ya Kanali Patrick Karegeya, aliyewahi kuwa mkuu wa idara ya Ujasusi ya Rwanda.Wanda-ma-naji wamedai kuwa serekali ya Rwanda imehusika na kifo hicho kilichotokea mwezi uliopita.

Karegeya alipatikana akiwa amefariki dunia katika hoteli moja mwezi Disemba mwaka uliopita.

Wanaharakati wa upinzani kutoka Rwanda wanaoishi uhamishoni wamedai kuwa serikali ya Rais Paul Kagema huenda ndio iliyohusika na mauaji ya bwana Karegeya.

Ubalozi wa Rwanda nchini Afrika Kusini ulisema kuwa maandamano ya aina yoyote sio tisho kwa serikali ya Rais Kagame.

Karegeya alikuwa mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Rwanda, na alipatikana amenyongwa katika hoteli moja mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Mjane wa Karegeya amesema kuwa atazikwa nchini humo.

Taulo iliyokuwa na damu ilipatikana katika chumba ambapo maiti ya Karegeya ilipatikana na polisi wanaendelea kufanya uchunguzi. Hata hivyo hakuna mshukiwa yeyote aliyekamatwa.

Muaji ya Karegeya, yamesababisha madai dhidi ya serikali ya Rais Kagame kusema kuwa huenda ilihusika na mauaji hayo.

Karegeya alikuwa mshirika wa karibu sana wa Kagame kabla ya kutofautiana naye.