Waziri mkuu wa Tunisia ang'atuka

Image caption Ali Larayedh amekubali kuondoka mamlakani ili kuendeleza mageuzi ya demokrasia

Waziri mkuu wa Tunisia, Ali Larayedh, amejiuzulu ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kuendeleza mageuzi ya demokrasia nchini humo.

Anakabidhi madaraka kwa serikali ya mpito kama sehemu ya makubaliano yaliofikiwa mwaka jana kati ya chama tawala cha kiislamu Ennahda na upinzani.

Hatua nyengine katika makubaliano hayo zimeshaidhiishwa huku bunge likipigia kura katiba mpya pamoja na kuteua maafisa wa tume ya uchaguzi katika matayarisho ya uchaguzi mpya.

Kuuawa kwa viongozi wawili wa upinzani mwaka jana kulichangia kuzuka ghasia Tunisia.

Waziri wa viwanda Mehdi Jomaa ndiye atashikilia wadhifa huo kwa muda kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Chama tawala cha Ennahda pamoja na upinzani vilikubaliana mwaka jana kuwa Jomaa ashikilie wadhifa wa Rais wa mpito hadi uchaguzi ufanyike.

Ennahda kilishinda uchaguzi wa kwanza mkuu baada ya aliyekuwa Rais wa muda mrefu, Zine al-Abidine Ben Ali kuondolewa mamlakani kwa mapinduzi ya kiraia mwaka 2011.

Hata hivyo, chama cha Ennahda kimekuwa na wakati mgumu kutawala nchi hiyo kwani kinakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa makundi hasimu ya kisiasa.