Waasi wadhibiti ulinzi wa Bentiu

Image caption Malefu wamekimbilia hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa nje ya Bentiu

Waasi nchini Sudan Kusini wameanza harakati za kuulinda vikali mji wa Bentiu ambao waliutwaa kutoka kwa serikali wakiwa na hofu ya majeshi ya Serikali kuupigania.

Mwandishi wa BBC nchini humo Alastair Leithead anasema kua waasi wameanza kuleta vifaru ndani ya mji huo wenye utajiri wa mafuta huku majeshi ya serikali yakiendelea kuukaribia mji huo.

Maelfu ya watu wametafuta hifadhi katika kambi moja ya Umoja wa Matifa viungani mwa mji wa Bentiu.

Takriban watu 1,000 wameuawa tangu mapigano kuanza tarehe 15 Disemba mwaka jana.

Takriban watu 200,000 wameachwa bila makao kutokana na mapigano Sudan Kusini.

Mgogoro huu ulianza baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani Riek Machar, kwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya utawala wake . Madai aliyoyakanusha vikali.

Bwana Machar ana kikosi cha karibia wapiganaji 10,000.

Naye Salva Kiir anatoka katika kabila la Dinka ambalo ndilo kubwa zaidi Sudan Kusini.

Lakini viongozi hao wawili wana watu wanaowaunga mkono kutoka makundi pinzani licha ya mgogoro huo kuwa na hisia za ukabila.

Huku mzozo ukiendelea kutokota Sudan kusini na katika Jamhuri ya Afrika ya kati, mataifa ya Afrika yameanzisha jitihada za kutafuta njia za kusuluhisha mizozo hiyo.

Mkutano unaoendelea nchini Chad ni jitihada ya hivi karibuni katika kujaribu kuutatua mzozo katika Jamhuri ya Afrika ya kati, huku wanadiplomasia wa Kiafrika wanaokutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa wakijaribu kuutatua ule wa Sudan kusini.

Wapiganaji katika nchi zote wanapuuza jitihada hizo, wapiganaji waliojihami hawaonekani kuwa na hamu ya kutafuta suluhu ya kisiasa na kufikia makubaliano.

Taasisi za kieneo na kimataifa zinahusika kwa kushindwa kuchukua hatua inayohitajika kwa kasi. Lakini yanaonekana kukabiliwa na kazi kubwa katika maeneo tofauti Afrika, yalioathirika na mizozo mipya na ya zamani huko Mali, Congo , Somalia, Jamhuri ya Afrika ya kati na sasa Sudan kusini.