Michel Djotodia aenda kuishi uhamishoni.

Image caption Aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,Michel Djotodia wakati akipunga mkono baada ya kufika mjini D`jamena kwenye kikao cha wakuu wa nchi za kanda ya Afrika ya Kati.

Aliyekuwa rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya kati, Michel Djotodia ameenda kuishi uhamishoni nchini Benin siku moja baada ya kujizulu wadhifa wake huo kufuatia shinikizo kutoka kwa viongozi wa kikanda wa eneo hilo kwa kushindwa kumaliza hali ya machafuko nchini humo.

Alikuwa ni rais wa kwanza Muislam kuiongoza nchi hiyo.

Nazo vurugu zimeendelea baina ya makundi ya wapiganaji kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.

Shirika la msalaba mwekundu limesema watu wapatao watatu wameuwawa kwa kupigwa risasi akiwemo raia mmoja-licha ya kutangazwa hali ya hatari na wtau kutotakiwa kutoka nje.

Walinda amani wa jeshi la Ufarnsa walirushiana risasi na wapiganaji.

Milio zaidi ya risasi imesikika asubuhi ya leo katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Kumekuwa na taarifa kuwa kuna matukio ya uporaji yamefanyika. Shirika la Uhamiaji limepanga kuhamisha wahamiaji wa kigeni ambao wamekwama nchini humo.