UN yamuasa Kiir kuwaachilia wafungwa

Image caption Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametishia kupeleka wanajeshi wake Sudan Kusini ikiwa Machar hatakubali kusitisha mapigano

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limemsihi Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir awaachilie huru wafungwa wa kisiasa ili aweze kumaliza mgogoro wa kisiasa unaotokota nchini humo.

Kiongozi wa waasi Riek Machar, anataka wafungwa 11 wa misiasa waachiliwe huru kabla ya kutia saini mkataba wowote wa Amani .

Majeshi ya Machar ambaye pia alikuwa makamu wa zamani wa Rais nchini Sudan Kusini, yanaonekana kushindwa hasa baada ya serikali kukomboa mji wa Bentiu ambao walikuwa wameuteka.

Serikali inasema inajiandaa kuukomboa mji wa Bor, ambao ni wa mwisho unaodhibitiwa na wanajeshi waasi wa Machar.

Machar amesema kuwa atajitahidi kuendelea kuudhibiti mji wa Bor ambao ni mji mkuu wa jimbo la Jonglei lililo umbali wa kilomita 200 Kaskazini mwa Juba.

Machar aliambia shirika la habari la AFP kuwa wapiganaji wake walishindwa katika mji wa Bantiu kwa sababu ilikuwa nia yao kuzuia vita kwa lengo la kulinda maisha ya Raia.

Msemaji wa jeshi Philip Aguer anasema kuwa pande zote zimepata hasara kwani baadhi ya wapiganaji wao wameuawa katika vita hivi ambavyo vingali kupata suluhu.

Maelfu walilazimika kuutoroka mji wa Bentiu wakati jeshi la serikali lilipokuwa katika harakati za kuukomboa.