Tamu, lakini unajua Madhara yake?

Image caption Baadhi ya kampuni huweka sukari hata katika bidhaa ambazo hazihitaji sukari mfano maji

Kikundi cha wanaharakati nchini Uingereza kimeanza juhudi za kutaka makampuni ya vyakula na vinywaji vya kuhifadhiwa kwenye chupa na mikebe kama Soda kupunguza kiwango cha sukari katika bidhaa zao.

Hii ni sehemu ya kampeini ya kutaka kukabiliana na tatizo la kiafya la unene kupita kiasi pamoja na ugonjwa wa kisukari nchini humo.

Kauli mbiu yao ni kuchukua hatua dhidi ya kiwango cha sukari kwenye chakula .

Kikundi hiki kimeanzishwa na wanaharakati walioanzisha harakati za kushurutisha makampuni kupunguza kiwango cha Chumvi katika vyakula vinavyohifadhiwa kwenye mikebe tangu mwaka 1990.

Wanaharakati hawa wanataka kuwajulisha watu kujizuia na vyakula vyenye sukari nyingi na kushurutisha wenye makampuni kupunguza sukari katika vyakula hivyo.

Image caption Baadhi ya vyakula vyenye sukari

Wanaamini kwamba makampuni yanaweza kupunguza bidhaa hiyo kwa asilimia 20 au 30 katika miaka mitano ijayo.

Aidha wanaharakati wanataka kuiwekea malengo sekta ya chakula kupunguza kiwango cha sukari hatua kwa hatua kiasi cha wateja kukosa kutambua tofauti yoyote katika ladha ya vyakula hivyo.

Sukari ni bidhaa ambayo hutumiwa sana katika vyakula vingi ikiwemo, mikate, soda, vyakula vya mkebe na katika vyakula vingine ambavyo hata havihitaji sukari.

Na ndio maana sio jambo la kushangaza kuwa soda moja ya mkebe ina vijiko saba vya sukari.

Maji, Yoghurt na vyakula vingine ambavyo hata havihitaji kuwa na sukari vinawekwa sukari.

Je hili ni tatizo kubwa katika mataifa ya Afrika Mashariki au watu wanapenda sukari tu bila kujua madhara yake? Tuma ujumbe wako kwenye ukurasa wetu wa facebook bbcswahili