Mpenzi wa Hollande alazwa hospitalini

Image caption Hollande na Vallerie

Mama wa taifa nchini Ufaransa Valerie Trierweiler amelazwa hospitalini baada ya vyombo vya habari nchini humo kudai kuwa Rais Francois Hollande ana mchumba wa kando.

Rais Hollande anaishi na Valerie ingawa hawajaoana rasmi.

Bi Valleeie alilazwa hospitalini Ijumaa kwa maagizo ya daktari ili aweze kupumzika , baada ya jarida la Closer kuchapisha picha za Rais Hollande na mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye Julie Gayet.

Bwana Hollande hakukanusha madai hayo ingawa aliteta vikali kuhusu vyombo vya habari kuingilia maisha yake binafsi.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Conservative, Jean-Francois Cope amesema kuwa taarifa hiyo imeharibu sifa ya Ufaransa kimataifa.

Image caption Gayet mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Rais Hollande

Bi Trierweiler anatarajiwa kuondoka hospitalini baadaye Jumatatu.

Hii leo Rais Hollande alitarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu uchumi wa nchi hiyo ingawa mambo yanaonekana yatabadilika kutokana na taarifa hizi kuhusu kashfa ya mapenzi inayomwandama Hollande.

Trierweiler na Hollande walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 1988 akiwa mwandishi wa habari wakati huo nayeHollande akiwa mbunge wa chama cha kisosholisti.

Kura za maoni zinaonyesha ushawishi wa Hollande kudidimia na kwamba ni 25% pekee ya watu nchini humo wana Imani naye.