Kisanga cha Gavana kumzaba mwanamke

Image caption Wanawake wanataka gavana Kidero achukuliwe hatua mara moja

Shirika moja la kutetea haki za wanawake mjini Naiorbi Kenya, Covaw,linataka Gavana wa Nairobi Evans Kidero akamatwe mara moja na kushitakiwa kwa kosa la kumzaba kofi mwanasiaaa mwanamke ambaye pia ni mwakilishi wa wanawake Bi Rachel Shebesh.

Shirika hilo linasema kuwa linalaani kabisa dhuluma za kijinsia na kwamba watuhumiwa wa vitendo vya dhuluma dhidi ya wanawake wanapaswa kufikishwa mahakamani.

Kidero alipata afueni Jumatatu baada ya Mahakama kuu kumzuia mwendesha mkuu wa mashitaka kumfungulia mashitaka ya kosa la kumshambulia mwanasiasa mwenzake.

Mwaka jana Kidero alimzaba kofi mwakilishi wa maswala ya wanawake wa jimbo la Nairobi Bi Rachel Shebesh.

Purukushani lilizuka baada ya Bi Shebesh ambaye ni mwanasiasa mashuhuri mjini Nairobi kwenda katika ofisi ya Kidero akiwa ameambatana na wafanyakazi wa baraza la jiji waliokuwa wanagoma wakidai nyongeza ya mishahara.

Gavana Kidero naye alikuwa amerejea kutoka kwenye mkutano na Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, alipokutana ana kwa ana na Shebesh na baadhi ya wafanyakazi wa baraza la jiji.

Hapo ndipo kukazuka sokomoko huku Kidezo akimzaba kofi Bi Shebesh mbele ya watu waliokuwa wameambatana nao.

Baada ya tukio hilo wanasisa hao waliandikisha taarifa kwa polisi huku Kidero akimlaumu Shebesh kwa kumshambulia.

Jumatatu, mahakama kuu ilimzuia mwendesha mashitaka mkuu Keriako Tobiko kumfungulia mashitaka Gavana Kidero, saa chache baada ya jaji katika mahakama hiyo kumruhusu Shebesh kumfungulia mashitaka Gavana Kidero.

Wanasiasa hao wawili walikosa kutatua kesi yao nje ya mahakama huku wakili wa Shebesh akisema kuwa mteja wake amesubiri bila jibu Kidero atimize matakwa yake.