CAR: Je vurugu zimekwisha?

Image caption Wakazi wanasema kuwa hali mjini Bangui imerejea kama kawaida

Hali ya utulivu imerejea katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui baada ya wiki kadhaa za ghasia za kidini huku benki na ofisi zikifunguliwa. Masoko pia yameanza kufurika watu.

Kiongozi wa mpito anasema visa vya watu kupora na kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi vimekwisha.

Makundi ya wapiganaji wa dini ya kiisilamu na wakristo yamekuwa yakizozana tangu mapinduzi ya kijeshi kufanyika nchini humo Mwezi Machi.

Asilimia 20 ya wakazi wa mji huo wametoroka vita huku mashirika ya misaada yakitahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu.

Mwandishi wa BBC mjini Bangui Piers Schofield anasema kuwa watu sasa wanahisi kuwa salama kiasi cha kuanza kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Katika wiki za hivi karibuni mapigano yamekuwa yakichacha na kuwalazimisha watu kusalia majumbani mwao.

Polisi sasa wamerejea katika barabara za mji kushika doria, wakati wenyeji wakisema kuwa mji huo unaonekana kuwa na shughuli nyingi , hali ambayo haijashuhudiwa tangu mwezi Machi mwaka jana.

Wadadisi wanasema kuwa kuna dalili ya mambo kuwa shwari tangu kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa mpito Michel Djotodia mwishoni mwa wiki.

Kiongozi wa mpito pamoja na spika wa bunge Alexandre-Ferdinand Nguendet amesema kuwa ghasia zimekwisha na hakuna tena vurugu wala mashambulizi ya kulipiza kiasi.

Wakazi wanasema kuwa mji wa Bangui haujakuwa na shughuli nyingi kama sasa tangu mwezi Disemba.