Misri: Kura ya katiba yaendelea

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Raia mmoja wa Misri akionyesha picha ya kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Sisi

Raia wa Misri wameendelea na upigaji kura ya maamuzi kwa siku ya pili ikiwa ni harakati za kupata katiba mpya tangu jeshi la nchi hiyo kuuangusha utawala wa Rais wa zamani Mohammed Morsi.

Jeshi la Misri linashinikiza kura ya ndiyo ili kuhalalisha kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa rais wa Misri Mohamed Morsi, aliyeondolewa madarakani mwezi Julai mwaka 2013.

Vituo vya upigaji kura vimekuwa vikifunguliwa saa tatu asubuhi huku vikosi vya ulinzi vikiimarishwa tangu siku ya Jumanne huku watu tisa wakiripotiwa kuuawa katika vurugu zilizotokea ambapo wengi wa waliouawa ni wafuasi wa Morsi.

Katiba mpya inayotarajiwa kupatikana nchini humo itachukua nafasi ya katiba ya zamani iliyopitishwa na Rais Morsi chini ya chama chake cha Muslim Brotherhood ambacho hivi karibuni kimetajwa kuwa ni kundi la kigaidi.

Wanajeshi wapatao 160,000 na polisi 200,000 wamesambazwa maeneo mbalimbali nchini humo kwa lengo la kudhibiti usalama.