Hoja ya wapiganaji wa kiisilamu Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kunawiri kwa makundi ya wapiganaji limekuwa swala sumbufu kwa mataifa ya magharibi

Maafisa wa ujasusi kutoka nchi za Magharibi wamezuru Damascus, Syria kwa mazungumzo kuhusu kupambana na makundi ya wapiganaji wa kiisilamu

Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Syria, Faisal Mekdad ameambia BBC kuwa tofauti zimeibuka kati ya maafisa wa usalama wa dola za Magharibi na wanasiasa wanaomshinikiza Rais Bashar kung’atuka.

Makundi ya wapiganaji wa kiisilamu yanayopinga serikali ya Assad,yameendelea kunawiri na kuzua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa kimataifa.

Maafisa wa serikali ya Syria wanatarajiwa kuhudhuria mazungumzo ya Amani mjini Geneva wiki ijayo.

Hata hivyo, kundi rasmi la kisiasa la Syria, (Syrian National Coalition,) bado halijaamua ikiwa litahudhuria mkutano huo.

Duru zinasema kuwa kukosekana kwa umoja miongoni mwa wapinzani wa Bashar Assad kumetatiza sana mataifa ya Magharibi.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na BBC, Bwana Mekdad alisema kwamba serikali nyingi za kimagharibi, hatimaye zimeelewa kuwa hakuna kiongozi mbadala kwa Rais Assad.