Ukraine kuanzisha mazungumzo ya kisiasa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maandamano nchini Ukraine

Rais wa Ukraine Viktor Yanukovych, amesema kuwa ataunda tume maalum ya kushirikisha pande zote husika zinazopigania mageuzi ya kisiasa nchini humo.

Ghasia za kisiasa nchini zimeendelea kwa majuma kadhaa.

Tangazo hilo limetolewa siku moja baada ya mapambano makali katika mji mkuu wa Kiev, ambako magari yaliteketezwa na grunedi za kuwatawanya waandamanaji kutumiwa wakati polisi wa kupambana na ghasia wakikabiliana na wapinzani wa Serikali.

Idadi kubwa ya watu wamejeruhiwa katika makabiliano hayo.

Kiongozi wa Upinzani, Vitali Klitschko, alisema kuwa amemwomba Rais ajiuzulu na kuitisha Uchaguzi Mkuu.

Marekani imetoa wito kusitishwa kwa vurugu mara moja. Mapigano yalianza nchini humo miezi miwili iliyopita, baada ya Rais wa Taifa hilo kupuuza mkataba wa biashara na Jumuiya ya Ulaya na badala yake kuimarisha uhusiano na Urusi.