Binyavanga:Mimi ni mpenzi wa jinsia moja

Image caption Wainaina Binyavanga

Mwandishi maarufu wa vitabu nchini Kenya, Binyavanga Wainaina, amejitokeza hadharani kuwa yeye hushiriki mapenzi ya jinsia moja.

Hii inamfanya Binyavanga kuwa mmoja wa waafrika mashuhuri kujitokeza hadharani.

Matendo ya kimapenzi kwa watu wa jinsia moja hayakubaliwi nchini Kenya, na nchi nyinginezo za Afrika.

Alifichua hali hii katika taarifa yake kupitia kwa mtandano wa kijamii wa Twitter iliyowiana na siku ya kuzaliwa kwake.Ana umri wa miaka 43.

Hii inakujia wakati ambapo kuna mjadala mkali nchini Kenya na katika baadhi ya mataifa ya Afrika kuhusiana na suala la haki za wapenzi wa jinsia moja.

Hivi karibuni, Nigeria ilipitisha sheria ambayo inatoa adhabu kali kwa makundi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, ilhali Rais wa Uganda alikataa kuhalalisha mswada kama huo uliopitishwa bungeni.

Uamuzi wa Binyavanga kujitokeza hadharani umepokelewa kwa hisia mbali mbali nchini Kenya. Kunao waliompongeza ingawa baadhi wanahisi kuwa huenda jamii ikamnyanyapaa.

Binyavanga aliwahi kushinda tuzo la mwanadishi bora zaidi Afrika la Caine mwaka 2002.

Watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja nchini Kenya wanaweza kuadhibiwa kifungo cha miaka kumi jela ikiwa watapatikana na hatia.