2 wauawa kwenye Ghasia Ukraine

Haki miliki ya picha AP
Image caption Makabiliano yameanza upya leo kati ya waandamanaji na polisi mjini Kiev

Watu wawili wameripotiwa kuuawa katika mji mkuu wa Ukraine Kiev katika makabiliano yaliyozuka upya kati ya polisi na waandamanaji wakati polisi walipovamia vizuizi vilivyowekwa na waandamanaji hao.

Waandamanaji hao walirusha mabomu ya petroli pamoja na mawe huku polisi wakijibu kwa kuwafyatulia risasi za mpira, maguruneti ya kuwaduwaza na gesi ya kutoa machozi.

Vurugu hizo zinajiri wakati sheria ya kupiga marufuku maandamano ya upinzani zikianza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo.

Kumeripotiwa ghasia chache usiku kucha mjini Kiev, baada ya vurugu kumalizika.

Vijana walikabiliana kwa mbali na polisi wa kupambana na ghasia walioshika doria nje ya majengo ya bunge. Wiki jana bunge la Ukraine lilipitisha sheria mpya kupiga marufuku maandamano ya hivi karibuni nchini humo.

Sheria hio imeweka kifungo cha miaka mitano kwa wote watakaopatikana wakizingira majengo ya bunge.

Pia ni hatia kuweka kizuizi bila kibali.Waziri Mkuu wa Ukraine Mykola Azarov ameonya kutumia nguvu ikiwa maandamano nchini mwake yataendelea.

Tayari mamia ya polisi na waandamanaji wamejeruhiwa kwenye makabiliano hayo. Baadhi ya waandamaji walipoteza macho baada ya kupigwa risasi za mpira.