Sheria ya ubakaji yarekebishwa-Morocco

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanaharakati wakipinga ubakaji nchini Morocco

Bunge nchini Morocco, limepiga kura kwa kauli moja kufanyia marekebisha sheria inayoruhusu wanaume waliowabaka wasichana kutofunguliwa mashitaka, ikiwa watawaoa waathiriwa wao.

Kura hiyo imepigwa takriban miaka miwili baada ya msichana mmoja mwenye umri wa miaka kumi na sita, Amina al-Filali, kujiua baada ya kulazimishwa kuolewa na mtu aliyembaka.

Wazazi wa msichana huyo na jaji mmoja, waliruhusu ndoa hiyo ili kulinda hadhi na heshima ya familia hiyo.

Kesi hiyo iliwashangaza watu wengi nchini Morocco mbali na kusababisha maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Rabat, na miji mingine mikubwa.

Wanaharakati wa kutetea haki za akina mama wameafiki mabadiliko kwenye kifungo hicho cha sheria.

Chini ya katiba ya nchi hiyo mtu aweza kuoa au kuolewa baada ya umri wa miaka kumi na minane.