IGAD kupeleka wanajeshi S. Kusini

Image caption Waasi wanaoongozwa na Riek Machar

Mataifa ya Afrika Mashariki yameidhinisha kupelekwa kikosi cha wanajeshi 5,500 nchini Sudan Kusini ili kumaliza mgogoro wa kisiasa ambao umekuwa ukiendelea kwa wiki kadhaa sasa.

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Amina Mohammed, amesema kuwa kamati ya usalama ya shirika la IGAD, imeidhinisha kikosi cha wanajeshi elfu tano kwenda Sudan Kusini kupambana na waasi.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine kuachwa bila makao huku wakikimbilia usalama wao kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya waasi wa Riek Machar na wanajeshi wa serikali ya Salva Kiir.

Shirika la IGAD linaendesha harakati za kupatanisha pande zinazozozana kwenye mgogoro huo ambao Umoja wa Mataifa unasema kuwa uhalifu dhidi ya binadamu umetendwa ikiwemo mauaji ya halaiki , dhuluma za kingono na uharibifu mkubwa.

Uganda ambayo ni mwanachama wa IGAD, tayari imetuma wanajeshi wake Sudan Kusini kivyake na kueleza wazi kuwa inasaidia wanajeshi wa Sudan Kusini dhidi ya waasi.

Kiongozi wa waasi, Riek Machar anataka serikali ya Uganda kuondoa wanajeshi wake kutoka Sudan Kusini akidai kuwa wanajeshi hao wamekuwa wakijaribu kumuua.

Amina amesema kuwa Kenya imeombwa kupeleka wanajeshi lakini bado inasubiri uamuzi kutoka kwa wakuu wa serikali.

Jeshi la Kenya lilitumwa Sudan Kusini vita vilipoanza ili kusaidia katika kuwahamisha raia waliokuwa wamekwama huko wakati vita vilipoanza.

Bi Amina amesema kuwa wanajeshi hao watasaidia katika juhudi za kuhakikisha kuwa vita vimesitishwa na hali kurejea kama kawaida.