Mkutano kuhusu Syria waanza-Uswizi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Katibu mkuu wa UN na mjumbe maalum wa Kimataifa nchini Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameambia pande mbili zinazozozana nchini Syria kuwa wakati umefika kwao kufanya mashauriano ya kusitisha mzozo unaokumba taifa hilo.

Akizungumza siku moja baada ya siku ya kwanza ya mkutano wa amani unaofanyika nchini Uswizi, Bwana Ban amesema kuwa lazima raia wa Syria waungane ili kuokoa taifa lao na kuwalinda watoto.

Awali, wajumbe wa Serikali na wale wa Baraza la Upinzani walikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza, tangu mzozo huo uanze miaka mitatu iliyopita.

Wajumbe hao walishutumiana, kuashiria mgawanyiko mkali kuhusu ikiwa rais Bashar al Assad, anapaswa kuwa na wadhifa katika serikali ya mpito.

Mabalozi wa mataifa ya magharibi wamesema kuwa uhasama huo unaweza kuhujumu, mazungumzo rasmi yatakayoanza siku ya Ijumaa.

Mjumbe wa wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Lakhdar Brahimi, amesema atashauriana na pande hizo mbili baadaye hii leo ili kujadili jinsi mazungumzo hayo yatakavyoendelea.

Balozi wa Syria, katika Umoja wa Mataifa Bashar Ja'afari amelalamika kuwa kumekuwa na mapungufu katika mazungumzo hayo kwa sababu ya kutokuwepo kwa Iran, nchi inayowaunga mkono kwa sababu wajumbe wengine wanaohudhuria mkutano huo ni wapinzani wa serikali.