Mkuu wa mageuzi ya polisi Kenya atishwa

Image caption Mkuu wa tume ya huduma kwa polisi nchini Kenya Johnstone Kavuludi

Polisi nchini Kenya wanachunguza chanzo cha barua ya vitisho kwa maisha ya mkuu wa tume ya huduma kwa polisi kuhusiana na shughuli inayoendelea ya kuwachuja maafisa wakuu wa polisi kuhusiana na utenda kazi wao.

Tume hiyo imekuwa ikiendesha shughuli hiyo kwa zaidi ya wiki tatu sasa.

Maafisa wa ujasusi wameanzisha uchunguzi kuhusu ilikotoka barua hiyo aliyotumiwa Kavuluzi Jumanne ikiwa na chembechembe za poda inayoaminika kuwa sumu.

Barua hiyo ilitumwa kwa mkuu huyo Johnston Kavuludi na kamishna mwingine wa tume hiyo Mohamed Murshid na kuwaonya dhidi ya kuwahoji vikali maafisa wakuu wa polisi.

Wameonya kuwa ikiwa hawatababadili wanavyoendesha mchujo huo, watakabiliwa na hatari kubwa.

Hadi sasa maafisa karibu watano wameachishwa kazi baada ya tume hiyo kuafikia kuwa utenda kazi wao una dosari chungu nzima.

Ujumbe huu unakuja huku tume hiyo ikitarajiwa kutangaza matokeo ya mchujo waliofanyia maafisa wakuu wa polisi ambapo waligundua ufisadi umekita mizizi katika idara ya polisi.

Barua hiyo iliyoandikwa kwa mkono ilitoa vitisho vya hatari kwa maisha ya Kavuludi na Murshid kuhusiana na mchujo wanaoendesha.

Mwaka jana Kichwa cha binadamu kilifikishwa katika ofisi za tume hiyo kikiwa na ujumbe kwa Bwana Kavuludi akitishiwa kuuawa.