Iran: Uchaguzi huru utaokoa Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Hassan Rouhani

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema kuwa Syria inahitaji uchaguzi huru na wa haki kama njia pekee ya kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unatokota nchini humo.

Ameyasema hayo kwenye mkutano wa kimataifa kiuchumi mjini Davos Uswizi.

Bwana Rouhani amesema kuwa watu wa Syria wanapaswa kujitengezea mustakabali mwema wao wenyewe,bila ya ushawishi wowote kutoka katika nchi za kigeni.

Kabla ya kutoa matamshi yake Bwana Rouhani alinukuliwa mapema wiki hii akisema kuwa mazungumzo ya Syria yatafeli,hasa baada ya Umoja wa Mataifa kufutilia mbali mwaliko wa Iran kwenye mkutano huo.

Umoja wa Mataifa ulisema kuwa Tehran ilikataa kuunga mkono wito wa kuundwa serikali ya mpito nchini Syria.

Mashauriano

Balozi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Lakhdar Brahimi, anatarajiwa atafanya mashauriano na makundi mbalimbali yanayozozana nchini Syria katika mkutano unaoendelea Uswizi.

Sherehe ya kufungua mkutano huo iliyofanywa Jumatano ilimulika tofauti kubwa zilizoko kati ya wajumbe wa Serikali na wa makundi ya waasi yaliyofika katika mkutano huo.

Bwana Brahimi amesema kuwa hajui kama wajumbe hao wako tayari kuketi katika chumba kimoja cha mkutano kufikia wakati huu. Lengo lake leo ni kupiga darubini jinsi makundi haya yalivyo tayari kufanya kazi pamoja na pia kuandaa mpango wa yatakayojadiliwa ifikapo hiyo kesho.

Anatazamia kutilia mkazo maswala kama vile hatua zinazopaswa kuchukuliwa kusitisha mapigano na nafasi kutolewa kwa mashirika ya kutoa misaada kuwafikia waathirika katika maeneo yote yanayoathirika na vita hivyo. Alisisitiza kuwa kwa sasa maswala ya kisiasa yataepukwa.