Polisi wakamatwa kwa mauaji A.Kusini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Polisi wakiwafyatulia risasi waandamanaji nchini Afrika Kusini

Polisi wanne wamekamatwa kuhusiana na kisa cha kuwapiga risasi waandamanaji nchini Afrika Kusini siku ya Alhamisi.

Tshepo Babuseng, mwenye umri wa miaka 28, alipigwa risasi na polisi katika maandamano kuhusu swala la makaazi viungani mwa mji wa Johannesburg.

Ripoti za awali, zilisema kuwa umati wa watu uliwavamia polisi waliokuwa wanaondoa vifusi barabarani. Hapo ndipo polisi mmoja alipowapiga risasi waandamanaji hao.

Mmoja wa maafisa hao anakabiliwa na tuhuma za mauaji wakati wengine wakikabiliwa na kosa la ukandamizaji.

Msemaji wa polisi katika mkoa wa Gauteng, amesema kuwa polisi hao walio na umri wa kati ya miaka 33-49 watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

Kitengo cha kuchunguza polisi kinasema kuwa kitafanya uchunguzi huru wa ndani kuhusiana na tuhuma hizo.

Kwa sasa polisi hao wameachishwa kazi kwa muda hadi kesi itakapoamuliwa.

Polisi nchini Afrika Kusini hutuhumiwa mara kwa mara kuhusu kuwatesa watu na kutumia njia zisizofaa kupambana na makundi ya watu wanaokuwa wanaandamana.

Mapema wiki hii kufuatia hatua ya polisi kuwapiga risasi watu wanne katika maandamano tofauti, waziri wa polisi Nathi Mthethwa aliambia BBC kuwa polisi watakawaua raia wasio na hatia hawatalindwa.

"polisi wanapata mafunzo kuwalinda raia na kuwahudumua. Hawafunzwi kuwaua,'' alisema waziri huyo.

Mwaka 2012, polisi waliwapiga risasi wafanyakazi 34 wa migodi waliokuwa wanagoma katika mgodi wa Marikana , tukio la kushangaza zaidi kuwahi kutokea tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi 1994.

Mwaka jana maafisa walinaswa kwa kanda ya video wakimfunga mwanamume kwenye gari kabla ya kumburura barabarani. Mwanamume huyo alipatikana akiwa amefariki.