Uhuru una maana gani?

Thailand ndio nchi ya tatu duniani inayoongoza kwa kusafirisha nje mazao ya baharini na inasambaza kwenye maduka makubwa nchini Marekani na katika nchi za Umoja wa Ulaya, EU.

Lakini inashutumiwa kwa kuwatumia mabaharia kutoka Burma na Cambodia ambao wameuzwa na kulazimishwa kufanya kazi kama watumwa.

Muziki wa kijeshi unasikika kwa sauti kubwa.

Mbele yetu wako maafisa wa polisi 100 wakiwa wamejipanga mstari. Jenerali Chatchawal Suksomjit, Naibu Mkuu wa Polisi, anapita karibu na askari waliojipanga akisalimiana nao na kupiga saluti.

Akiwa amevalia miwani yake myeusi na sare za kijivu anaashiria jambo muhimu. Anatuamuru kuelekea kwenye boti za polisi zinazosubiri kwenye mwambao wa Malacca karibu na mpaka na Malaysia.

Jenerali huyo ni mkuu mpya wa kamati iliyoundwa kushughulikia tatizo la usafirishaji wa wanaume kwenda kwenye biashara ya uvuvi, sekta anayoielezea kuwa ni ‘hatari, ngumu na isiyofaa’.

Haki miliki ya picha MCOT
Image caption Mitumbwi inayotumika kwa uvuvi

‘Tatizo kubwa tunaloliona ni kwamba, endapo watu hawatafanya kazi wanakuwa hawana maana ndani ya boti, wanaweza kuuawa na kutoswa baharini,” anasema. Haitokei katika kila boti lakini inatokea sana hivyo kuzua maswali mazito kuhusu kukosekana kwa sheria katika sekta hii.”

Pia kuna tatizo la uhaba wa ajira. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kazi, sekya uvuvi nchini Thailanda ina upungufu wa ajira 50,000. Nahodha mmoja katika bandari ya Chonburi anasema wanataabika.

Kimsingi, mfanyakazi haramu kutoka Cambodia au Burma hukutana na dalali na hupatiwa ajira ya kiwandani. Anaikubali na hujikuta akitambulishwa kutoka kwa dalali mmoja hadi mwingine, na kasha hupelekwa bandarini na kupandishwa ndani ya boti. Na baada ye huambiwa anadaiwa pesa nyingi.

Ni mtego wa hatari. Endapo atatoroka, kama mhamiaji asiyeandikishwa polisi watamkamata na kumrejesha kwao. Mwanaume mmoja kutoka Cambodia niliyezungumza naye alitumikishwa kwenye boti kwa miaka mitatu bila kulipwa ujira wake, akadanganya kuwa pesa yote kalipa madeni. Hakuwahi kuambia kiasi anachodaiwa.

Jenerali na wasaidizi wake hawawezi kuzungumza moja kwa moja na baharia wa Burma kwa sababu hawajaleta mkalimani hivyo inawawia vigumu kutambua kama watu hao wamesafirishwa kiharamu.

“Si ingekuwa kazi rahisi kama mngekuwa na mkalimani?” Nauliza. Anajibu kwa kawaida wanategemea mtu anayekuwepo ndani ya boti ambaye anaweze kuzungumza lugha ya Burma, kama nahodha pengine. Hata hivyo, mara nyingi ni nahodha ndiye anayetuhumiwa kwa unyanyasaji na utesaji.

‘Ni kwa vipi mnaweza kutambua kwamba, hapa hakuna watu waliosafirishwa kiharamu ama kulazimishwa kufanya kazi?’ Nauliza tena.

‘Kwa jinsi tulivyoshuhudia, hakuna chumba wala mahabusu ya kuwahifadhi watu wanaokamatwa,’ anasema. ‘Hatukuona alama zozote za majeraha kwenye miili yao ama nyuso zao. Kwa kuangalia nyuso zao na macho hawaonekani kama walilazimishwa kufanya kazi.’

Wakati mamlaka inapowaokoa watu waliosafirishwa kiharamu, mara nyingi huwahifadhi katika kituo cha serikali nje ya mji mkuu wa Bangkok.

Ken ni mmoja wa watu hao. Anaeleza kwamba, aliahidiwa kazi nzuri ya kiwandani lakini akalazimishwa kupanda boti ndogo baharini ambako alifanya kazi ya uvuvi kwa saa 20 kwa siku, siku saba za wiki. Dalali anasema kwamba, Ken alikuwa akidaiwa fedha nyingi baada ya kupatiwa ajira na kupelekwa bandarini. Miezi ikapita na Ken, kama walivyo wengine wengi hakulipwa pesa yake.

‘Watu wanasema, yeyote anayejaribu kutoroka huvunjwa miguu yake na mikono ama hata kuuawa,’ Ken anasema .

Image caption Samaki wengi wanaotoka Thailand

Akihangaika kutoroka, Ken alijitosa baharini na kuogelea kwa saa sita , hadi alipookolewa na boti nyingine na kushushwa karibu na mwambao wa Pattaya. Kama ilivyo kwa wanaume wengi kama yeye, alijisikia aibu kurejea nyumbani akiwa mikono mitupu, hivyo polisi walipomkamata na kumrejesha nyumbani alivuka mpaka tena na kurejea Thailand kusaka ajira.

Naibu Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Kazi, Puntrik Smiti, anakiri kwamba, wanaume kama Ken wako hatarini. ‘Kuna baadhi ya makampuni ya uvuvi ambayo yanajaribu kuboresha maslahi ya wafanyakazi wao,’ anasema. ‘Tatizo ni kwamba, kuna makampuni madogo ambayo hayajasajiliwa na hayataki kuingia kwenye mfumo huo.’

Kadhalika anabainisha kuwa, sheria za ajira zilizopo hazijitoshelezi. Kimsingi, Sheria ya Thailand ya Kulinda Ajira haiwahusu wafanyakazi walioajiriwa katika sekta ya uvuvi, wakati sheria nyingine za wizara haziyahusu maboti yenye mabaharia chini ya 20, ama yale yanayosafiri nje ya eneo la maji ya Thailand kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Siku chache baada ye tuko Burma, tumekaa sakafuni kwenye nyumba ya mianzi huko Bago kilomita 100 kaskazini ya mji mkuu Rangoon. Hapa ni nyumbani kwa Ken. Ingawa panaridhisha lakini hali ya umasikini ni dhahiri.

Wazazi wa Ken hawajasikia lolote kwa miaka minne, kutoka kwa mtoto wao ambaye sasa ana miaka 32.