Upinzani waungana Afrika Kusini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Dr Mamphela Ramphele hana ufuasi mkubwa sana nchini Afrika Kusini licha ya sera zake kupendwa

Chama rasmi cha upinzani nchini Afrika Kusini,(Democratic Alliance) kimemtangaza Dr Mamphela Ramphele ambaye pia alikuwa mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi kuwa mgombea wake wa uchaguzi mkuu mwezi Aprili.

Bi Ramphele, aliyekuwa mwandanani wa mpigania uhuru Steve Biko, aliunda chama chake cha kisiasa cha Agang mwaka jana.

Kiongozi wa chama cha Democratic Alliance, Helen Zille alisema hakuna mwanasiasa mwingine mwenye uwezo wa kutawala nchi hiyo kama Bi Ramphele.

Wadadisi wanasema kuwa hatua hii inalenga kuondoa tuhuma kuwa chama cha DA kina ufuasi mkubwa wa waafrika wazungu na kwamba hakiwezi kupata ushindi kwa hilo.

Viongozi hao wawili walisema kuwa kuungana kwao kutaleta umoja miongoni mwa wananchi Afrika Kusini , umoja ambao marehemu Mandela alipigania.

Bi Ramphele, mwenye umri wa miaka 66, anaonekana kama mtu mwenye ajenda nzuri na pia anasifika kwa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi baadhi ya mambo ambayo yanawashawishi watu kupiga kura.

Hata hivyo, chama chake cha Agang, kimekosa kuwa na ushawishi tangu kizinduliwe mwaka jana.

Mwezi jana Chama cha Agang kilikabiliwa na changamoto ya fedha kiasi cha kutoweza kuwalipa wafanyakazi wake.

Mwandishi wa BBC Milton Nkosi mjini Johannesburg anasema kuwa muungano huo bila shaka utachangamsha uchaguzi mkuu mwaka huu ingawa chama tawala cha ANC kinatarajiwa kusalia kuwa na ushawishi mkubwa.

Anasema kuwa Rais Jacob Zuma huenda akasalia madarakani licha ya kashfa nyingi za ufisadi zinazokumba chama tawala ANC.