Msako dhidi ya raia wa kigeni Kenya

Haki miliki ya picha AP
Image caption Tisho la igaidi ndilo limesababisha polisi kufanya msako dhidi ya raia wa kigeni walio Kenya kinyume na sheria

Polisi nchini Kenya wamewakamata mamia ya raia wa kigeni mjini Nairobi huku msako mkali ukiendeshwa dhidi ya watu wanaoshukiwa kuwa nchini humo kinyume na sheria.

Naibu msemaji wa polisi Zipporah Gatiria Mboroki , amesema kuwa polisi waliendesha msako huo katika mitaa kadhaa ikiwemo mtaa wa Eastleigh, ambako wanaishi wasomali wengi wenye asili ya kisomali na kikenya.

Katika miaka ya hivi kribuni, mtaa wa Eastleigh umeshuhudia ongezeko la wafanyabiashara wa kisomali waliotororoka vita nchini Somalia.

Eneo hilo pia limekuwa kitovu cha uhalifu huku mashambulizi kadhaa ya kigaidi yakitelezwa katika mtaa huo, huku silaha ndogondogo zikizagaa.

Mwezi mmoja uliopita, hali ya usalama iliimarishwa katika miji kadhaa nchini humo baada ya kutokea shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Westgate na kusababisha vifo vya watu zaidi ya sitini.

Wakazi wa Eastleigh wanasema kuwa polisi wamekuwa wakiendesha msako dhidi ya watu wasio na vyeti halali vya kuishi nchini humo kwa wiki kadhaa sasa.

Mkazi mmoja katika mtaa huo alisema kuwa polisi huwakamata zaidi ya watu hamsini, kuwahoji na kisha kuwaachilia baadhi huku wengine wakiishia kuzuiliwa.

Hata hivyo raia wa kisomali wamekuwa wakilalamika kuwa polisi huwalenga kuwakamata kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Lakini polisi wamekuwa wakitetea msimamo wao wakisema kuwa ni watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab pekee ambao hukamatwa.

Mnamo siku ya Alhamisi, balozi kadhaa nchini kenya zilitoa tahadhari kwa raia wa nchi zao kuwatahadhari kutokana na tisho la shambulizi la kigaidi nchini Kenya.

Hatua ya kukamatwa kwa raia hao wa kigeni imekuja siku mbili baada ya polisi kukamata polisi mmoja na mfanyakazi mmoja wa shirika la ndege kwa kumiliki hati bandia za usafiri.

Raia waliokamatwa ni kutoka Ethiopia, Somalia na Bangladesh.