Morsi afikishwa mahakamani Misri

Haki miliki ya picha AP
Image caption Morsi akiwa kizimbani kujibu mashtaka

Aliyekuwa Rais wa Misri Mohammed Morsi amefikishwa mahakamani kwa mara nyingine kujibu tuhuma anazokabiliwa nazo.

Morsi aliwasili mahakamani mjini Cairo kwa kutumia helikopta ya jeshi kutoka gereza anakozuiliwa mjini Alexandria.

Bwana Morsi na washirika wake 14 wa vuguvugu la Muslim Brotherhood wameshtakiwa kwa kosa la kuchochea mauaji ya waandamanaji nje ya ikulu ya Rais mnamo mwaka 2012.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi yake siku nne zilizopita ,bwana Morsi alipuuzilia mbali mashtaka dhidi yake na kukana uhalali wa mahakama huku akisema kuwa bado yeye ndiye rais halali wa taifa hilo aliyechaguliwa na raia.

Aling'atuliwa mamlakani na jeshi mnamo mwezi Julai mwaka uliopita baada ya kundi kubwa la raia kumkana.

Mnamo siku ya Ijumaa polisi wa kupambana na ghasia walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa Mosri mjini Cairo na Alexandria pamoja na Fayoum kusini mwa mji mkuu .