Karzai awatusi wanajeshi waliouwawa

Wanajeshi wa Uingereza wakitua Helmand Kusini, Afghanistan Haki miliki ya picha GETTY IMAGES

Mzazi wa mwanajeshi wa Uingereza aliyeuwawa nchini Afghanistan amemshutumu Rais Karzai kuwa amelitemea mate kaburi la mtoto wake kwa kusema, kama inavoarifiwa, kwamba jimbo la Helmand lingekuwa afadhali ingekuwa wanajeshi wa Uingereza hawakuingia huko.

Jacqui Janes alisema matamshi ya Bwana Karzai katika mahojiano na gazeti la Sunday Times, ni tusi kwa kila mtu aliyepoteza maisha yake nchini Afghanistan.

Katika mahojiano hayo Rais Karzai alisema jeshi la kimataifa liloongozwa na Marekani, halikufanikiwa kuleta usalama, hasa katika jimbo la Helmand.

Wanajeshi 447 wa Uingereza wameuwawa Afghanistan tangu mwaka 2001, na zaidi ya 2,000 wamejeruhiwa.

Na kampeni za uchaguzi wa rais wa Afghanistan zimeanza leo, miezi miwili kabla ya kumchagua mrithi wa Rais Karzai.

Rais Karzai alichaguliwa mwaka wa 2001 na hawezi kugombea muhula wa tatu.