Nigeria kutumia ndege dhidi ya Boko.H

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jeshi limekuwa likipambana na Boko Haram kwa karibu miaka 5

Serikali ya Nigeria, inasema kuwa inapanga kununua ndege tatu maalum za kufanyia uchunguzi na kufuatilia shughuli za kundi la wapiganaji wa kiisilam la Boko Haram.

Waziri wa mambo ya ndani Abba Moro, amesema kuwa ndege hizo zitatumiwa, kufuatilia shughuli za Boko Haram mipakani,kusaka wahalifu na wahamiaji haramu.

Waziri Abba Moro amesema kuwa ununuzi wa ndege hizo ni mojawapo ya mbinu za serikali kupambana na ugaidi pamoja na utovu wa usalama unaochochewa na kuingia nchini humo kwa wahamiaji wasio na vibali.

Mwandishi wa BBC nchini Nigeria, anasema kuwa maafisa wa utawala wanafanya mazungumzo na serikali jirani ya Cameroon ili kuwezesha Nigeria kuvamia kambi za Boko Haram nchini humo.

Maelfu ya watu nchini Nigeria wameuawa tangu Boko Haram kuanzisha uasi nchini humo miaka mitano iliyopita.