Kundi la Taleban laondoka mazungumzoni

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Taleban yalaumu serikali kwa kuchelewesha mazungumzo

Wawakilishi wa kundi moja la wapiganaji wa Taleban nchini Pakistan ambao wako katika mazungumzo ya amani wamekasirika baada ya ujumbe wa serikali kudinda kuhudhuria mazungumzo ya awali.

Mjumbe mmoja wa kundi hilo ameitaja hatua hiyo kama njama ya serikali kuchelewesha mazungumzo hayo huku akionya kuwa 'chochote chaweza tokea kwa sasa'.

Ujumbe huo tayari umeondoka katika mji mkuu wa Islamabad.

Awali,wazungumzaji waliokuwa wakiiwakilisha serikali walilitaka kundi hilo kuelezea ni akina nani waliokuwa katika kundi lao.

Waandishi wanasema kuna wasiwasi kuhusu matarajio ya mazungumzo hayo kwa kuwa kundi la Taleban linasisitiza kuhusu kuidhinishwa kwa sheria za kiislamu pamoja na kuachiliwa huru kwa wafungwa wote wa Taleban.

Kundi la Taleban kutoka Pakistan lina mchanganyiko wa wanamgambo wa kiislamu wenye itikadi kali ambao wanataka kuanzisha utawala wa kiislamu.