Misururu ya mashambulizi yatikisa Iraq

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiganaji wa kiisilamu wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara Iraq

Watu 24 wameuawa katika msururu wa milipuko ya mabomu katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Mashambulizi hayo yametokea leo asubuhi wakati wa shughuli nyingi karibu na eneo lenye ulinzi mkubwa la Green Zone ambako ofisi nyingi za serikali zipo.

Mabomu mawili yaliyotegwa ndani ya gari yamelipuliwa nje ya wizara ya mashauri ya nchi za kigeni huku mlipuko mwingine ukitokea kwenye mkahawa.

Inaarifiwa washambulizi walipanga vyema kuhakikisha kuwa wanalenga maslahi muhimu waliyotaka.

Shambulizi la kwanza lililenga mkahawa ambao hutembelewa sana na wafanyakazi wa serikali ,wanajeshi na maafisa wa usalama.

Shambulizi la pili la bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari, lilitokea nje ya wizara ya mambo ya ndani wakati wafanyakazi na raia wa kawaida walipokuwa wamepanga foleni katika eneo lenye kizuizi .

Iraq imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni wakati wanamgambo wa kusini wenye uhusiano na al-Qaeda wakiendelea kudhibiti miji katika jimbo la Anbar.

Wametishia kupeleka vita vyao katika mji mkuu Baghdad hadi pale serikali itakapokubali kusitisha vita dhidi yao.