Familia kuunganishwa tena Korea

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wajumbe wa Korea Kaskazini na Kusini wakati wa mkutano wa kuziunganisha familia

Korea Kaskazini na Kusini zimekubaliana kuandaa shughuli ya kuwakutanisha watu wa familia zilizotenganishwa na vita vya Korea miaka sitini iliyopita. Shughuli hiyo itaandaliwa baadaye mwezi huu. Tangazo hilo limetolewa baada ya mazungumzo ya haraka yaliyofanyika baina ya Korea hizo mbili katika kijiji cha mpakani cha Panmunjom.

Baada ya mazungumzo kadhaa yaliyofanyika kwa kifupi, mengine yakidumu dakika chache tu, mpango wa kuwakutanisha mamia ya watu wa familia zilizotenganishwa umefufuliwa tena. Pande zote mbili zitafanya kazi ya kuziunganisha familia hizo katika eneo la milima ya Geumgang, Korea Kaskazini. Ni tukio lisilo la kawaida kwa Korea hizo mbili kushirikiana katika rasi hiyo baada ya miaka mingi ya uhasama.

Zaidi ya familia watu alfu 70,000 waliopoteana na jamaa zao wanaishi Korea Kusini na wengi wao kwa sasa wana umri wa zaidi ya miaka 80.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Raia wa Korea Kusini wanaosubiri kukutana jamaa zao wa Kaskazini

Wengi wao hawajapata kuwaona jamaa zao wa Korea Kaskazini tangu vita vya Korea.

Rais Wa Korea Kusini alielezea umuhimu wa kutekeleza zoezi hilo la kuunganisha jamaa za watu hao katika hotuba yake ya mwaka mpya. Na mwezi uliopita, Korea Kaskazni ilianza kuisihi Kusini kukomesha vitendo vya uhasama lakini wengi hawaamini kama uhusiano mzuri utaweza kupatikana kwa urahisi.

Mwandishi wa BBC aliyepo mjini Seoul anasema zoezi la kupatanisha familia hizo lilifutiliwa mbali na Korea Kaskazini na huku mazoezi makubwa ya kijeshi yakitarajiwa kuanza Korea Kusini baadaye mwezi huu, wengi wanajiuliza iwapo hali ya kuimarisha uhusiano kwa sasa itadumu.