Wanajeshi wamuua muasi wa Seleka CAR

Haki miliki ya picha c
Image caption Waasi wa Seleka

Wanajeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamemuua mwanamume mmoja anayetuhumiwa kuwa muasi huku ghasia zikiendelea kukithiri nchini humo.

Mwanamume huyo alidungwa kisu na kuchapwa kisha mwili wake ukateketezwa katika mji mkuu Bangui

Tukio hilo limesemekana kutokea baada ya Rais wa mpito Catherine Samba-Panza kumaliza hotuba yake katika hafla moja ya kijeshi.

Taarifa zaidi zinasema kuwa waasi wa Seleka wanajipanga upya Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Wapiganaji hao wanasemekana kuhusika na mashambulizi mapya dhidi ya raia.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch limesema wanajeshi kadhaa wa serikali ya Chad wanawaunga mkono waasi wa Seleka katika Jamhuri ya Afrika ya kati.

Shirika hilo linasema wanajeshi hao wa Chad wanaongoza shughuli za kundi la Seleka linaloshutumia kuwashambulia raia.

Chad ni mojawapo ya nchi inayochangia wanajeshi kwa ujumbe wa Umoja wa Afrika unaosaidia katika harakatiu za amani katika mji mkuu Bangui.

Jamuhuri ya Afrika ya Kati ni moja ya nchi za Afrika zinazokumwba na umaskini na tangu mapinduzi ya kijeshi kufanyika mwaka jana nchi hiyo imetumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Maelfu ya watu wameuawa tangu hapo.

Ghasia kati ya kundi la waasi wa Seleka ambao ni waisilamu na wakristo wanaojulikana kama 'anti-balaka' zimeendelea licha ya Rais Samba-Panza kuapishwa mwezi jana.

Kiongozi wa Seleka Michel Djotodia alijiuzulu kama Rais wa mpito, kama sehemu ya juhudi za kikanda kurejesha uthabiti katika nchi hiyo.