Umoja wa Mataifa waahidi misaada Syria

Haki miliki ya picha bbcpersian
Image caption Valerie Amos, mkuu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa

Mkuu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa Valerie Amos amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kimataifa hayatazuiwa kuendelea kutoa misaada nchini Syria kufuatia shambulio la Jumamosi katika msafara uliokuwa ukipeleka vyakula katika mji wa Homs.

Bi Amos amesema amesikitishwa sana na mashambulio hayo ambayo yamevunja makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku tatu ili kuruhusu misaada kupelekwa katika maeneo ya mji wa Homs.

Matukio hayo ni kielelezo cha hatari zinazowakabili kila siku raia na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada nchini Syria, amesema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa.

Bi Valerie Amos amesema Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo katika kufikisha misaada kwa wahitaji, lakini lazima wahakikishiwe usalama.

Msafara wa Umoja wa Mataifa ulishambuliwa kwa makombora na bunduki wakati ukiondoka Homs, Jumamosi, ikiwa ni siku ya pili ya kusitisha mapigano ili kuruhusu misaada kuwafikia watu wanaohitaji.

Serikali ya Syria imevilaumu vikundi vya waasi kutokana na shambulio hilo, lakini nao waasi wamesema majeshi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad yamehusika na shambulio hilo na kuchelewesha shughuli za usambazaji misaada Jumamosi asubuhi.