Hofu ya uhaba wa chakula CAR

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mamia ya waisilamu wamekuwa wakirotoka CAR kwa kuhofia maisha yao

Mashirika ya kutoa misaada yameonya kuwa endapo raia wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati ambao ni Waislamu, wataendelea kuihama taifa hilo, masoko ya nchi hiyo huenda yakasambaratika kabisa.

Mashirika ya kutoa misaada ya Oxam na lile la Action against hunger yamesema kuwa chini ya maduka kumi ya jumla ndiyo yalisosalia katika mji mkuu wa nchi hiyo na kuwa wafanyabiashara wengi wanaendelea kutoroka taifa hilo.

Kufuatia hali hiyo mashirika hayo yameonya kuwa chakula kinapungua kwa kiasi kikubwa na kuwa bei ya vyakula huenda ikapanda zaidi.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya asilimia tisini ya raia wa nchi hiyo, wanaishi kwa kula chakula mara moja kwa siku na kuwa hali hiyo huenda ikawa mbaya zaidi.

Taifa hilo limegawanyika zaidi kufuatia vita vilivyoanza mwaka uliopita kati ya Wakristu ambao ni wengi nchini humo na Waislamu kufuatia mapinduzi ya serikali.

Maelfu ya Waislamu tayari wametoroka nchini humo na kutafuta hifadhi katika mataifa jirani ya Cameroon na Chad.

Upungufu wa chakula

Kwa sasa kuna upungufu mkubwa wa nyama kwa sababu wafugaji wamekimbilia msituni na wakati wanapochinja mifugo wao, bei huwa ghali mno.

Wengi wa Waislamu waliofukuzwa na Wakristu walikuwa wakichangia pakubwa katika uchumi wa taifa hilo.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa huku ikiwa imesalia chini ya mwezi mmoja kabla ya msimu wa upanzi, zaidi ya asilimia tisini na sita ya wakulima hawana mbegu.

Ghasia zinazoendelea zimezuia vyakula kuingizwa nchini humo na ripoti zinasema kuwa mamia ya malori yaliyosheheni chakula yamekwama katika mpaka wa nchi hiyo na Cameroon, kwa sababu madereva wengi wana wasi wasi wa kushambuliwa na makundi yaliyojihami.

Shirika hilo la Oxfam, limesema kuwa endapo raia waliosalia hawatapewa ulinzi wa kutosha, hali nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati huenda ikawa mbaya zaidi.