Waasi wasusia mazungumzo ya amani

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Wajumbe wanaohudhuria mkutano wa amani mjini Addis Ababa

Waasi nchini ya Sudan Kusini wamesema kuwa hawatashiriki katika awamu ya pili ya mazungumzo ya kuleta amani yaliyokuwa yamepangiwa kuanza siku ya Jumatatu katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Waasi hao wamesema kuwa hawatarudi kwenye meza ya mazungumzo hadi wafungwa wanne wa kisiasa waliobakia watakapoachiliwa huru.

Aidha wawakilisha wa waasi hao wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa zamani wa Sudan Kusini, Riek Machar, wamesema mbali na wafungwa hao kuachiliwa huru, wao pia wanataka jeshi la Uganda ambalo limekuwa likiunga mkono serikali kuondoka nchini humo, kabla ya mazungumzo hayo kuendelea.

Mazungumzo hayo yanalenga kumaliza mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu tangu yalipoanza Desemba mwaka jana.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr amemshutumu makamu wake wa zamani kwa kuongoza uasi ndani ya serikali na kutaka kufanya mapinduzi ya serikali, madai ambayo yamepingwa vikali na Bwana Machar.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa mamia ya watu wameuawa tangu mapigano hayo kuanza huku maelfu ya wengine wakilazimika kuhama makwao na wanahitaji misaada.