Msako dhidi ya Mafia wanasa 26

Image caption Bandari Gioia Tauro iliyolengwa kutumika na Mafia

Polisi nchini Italia na Marekani wamefanya uvamizi unaofuatana katika nchi hizo mbili kama sehemu ya msako dhidi ya makundi ya mafia na wamewakamata watu 26.

Nchini Italia polisi wamewakamata wafuasi wa kundi la 'Ndrangheta ambao ni sehemu ya kundi la Mafia lililopo katika eneo la Calabria.

Nane walionaswa mjini New York wanahusishwa na kundi la Gambino huku 18 waliokamatwa nchini Italia wakishirikishwa na kundi la Mafia la Ndrangheta .

Maafisa wa usalama katika mataifa hayo wanasema watu hao walikamtwa kama sehemu ya msako dhidi ya biashara ya madawa yakulevya na kujipatia fedha na mali kwa njia haramu.

Operesheni hiyo inafuatia upelelezi wa miaka miwili iliyofanikisha kukamatwa kwa mamia ya kilo za mihadarati aina ya heroin na bangi iliyofichwa katika shehena ya matunda na nazi .

Madawa hayo yaliyonaswa yanasemekana yalikuwa yanaelekea katika bandari ya Gioia Tauro, moja ya bandari kubwa zaidi barani Ulaya .