Sudan:K:Duru ya pili ya Mazungumzo

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Licha ya mazungumzo kuanza, kuna tetesi kuwa vita vingali vinaendelea

Duru ya pili ya mazungumzo ya amani kati ya waasi na serikali nchini Sudan Kusini imeanza mjini Addis Ababa Ethiopia.

Awamu ya kwanza ya mazungumzo hayo ilikamilika baada ya pande zinazozozana kutia saini mkataba wa kusitisha vita mwishoni mwa mwezi Januari.

Hata hivyo pande hizo mbili zimetuhumiana kwa kukiuka mkataba huo.

Ajenda ya mkutano huo ni mazungumzo ya kisiasa na maridhiano ya kitaifa.

Waasi wamekuwa wakitaka serikali kuwaachilia makundi mawili ya wafungwa wa kisiasa waliokamatwa baada ya kutuhumiwa kwa kosa la uhaini.

Wafungwa saba waliachiliwa na sasa wako nchini Kenya ingawa wanne wangali wanazuiliwa nchini Sudan Kusini.

Pia wanataka wanajeshi wa Uganda kuondoka nchini Sudan Kusini ambako wanasaidia majeshi ya serikali kupambana na waasi.