Hatimaye msaada wawasili CAR

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mamia ya watu wansubiri kupokea chakula katika kituo kimoja mjini Bangui

Shirika la chakula duniani limesema kuwa ndege inayobeba chakula cha msaada kwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, imewasili mjini Bangui.

Tayari tani 82 za Mchele zimeingizwa nchini humo kutoka nchi jirani ya Cameroon.

Shirika hilo, linatarajia katika mwezi mmoja ujao, kuweza kulisha karibu wakimbizi laki moja na hamsini.

Chakula kingine cha tani 1,800 kitapelekwa nchini humo mwezi ujao.

Hata hivyo, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni moja nchini humo wanahitaji chakula.

Mapigano yameendelea kuchacha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutatiza shughuli ya kuingiza chakula nchini humo kwa kutumia barabara.

Wakati huohuo, walinda amani wamekosa kuzuia mauaji ya waisilamu. Hii ni kwa mujibu wa shirika moja la kutetea haki za binadamu.

Mashambulizi yanayofanywa na wapiganaji wakristo yamesababisha msururu wa waumini wa kiisilamu kutoroka nchini humo kutafuta hifadhi katika nchi jirani.

Mashirika ya misaada yametoa tahadhari ya uhaba wa chakula kutokana na maduka yaliyokuwa yanamilikiwa na wasilamu kufungwa.

Wakati huohuo,Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, amewasili nchini humo , kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kujaribu kumaliza ghasia katika taifa hilo.

Wanajeshi 1600 wa Ufaransa wapo nchini humo kama sehemu ya kikosi cha kimataifa cha kulinda amani.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon ameiomba serikali ya Ufaransa kuongeza kikosi chake katika Jamhuri ya Afrika ya kati kuzuia kugawanyika kwa taifa hilo na kuwepo maeneo ya waisilamu na wakristo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International linasema walinda amani wa kimataifa wameshindwa kuzuia mauaji hayo.