Mapigano yashika kasi Syria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakazi wa mji wa Homs wakiondoka kufuatia mapigano

Wanaharakati nchini Syria wameripoti kuwa mapigano yameshika kasi nchini humo wakati ambapo mazungumzo ya kufikia makubaliano ya kumaliza mapigano yakiendelea mjini Geneva.

Wanaharakati hao wamesema zaidi ya watu 200 wamekuwa wakiuawa kila siku kwa kipindi cha majuma matatu yaliyopita.

Vikosi vya Serikali na waasi wamekuwa wakipambana ili kuyashikilia maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, huku wanaharakati hao wakisema hali hiyo inajitokeza pengine lengo kuu ni kusisitiza misimamo yao katika mazungumzo ya Geneva.

mazungumzo kati ya serikali ya Syria na makundi ya upinzani yanaendelea nchini Switzerland lakini hakuna ishara yeyote ya kufikiwa kwa makubaliano.

Zaidi ya watu 200 waliondolewa kutoka mjini Homs, lakini mamia wameendelea kukwama mjini humo.

Mapigano ya nchini Syria yamegharimu maisha ya watu zaidi ya 100,000 huku wengine milioni 9.5 wakiyakimbia makazi yao.