Mlipuko wa bomu wasababisha vifo-Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Gari lililolipuka mjini Mogadishu

Takriban watu sita wameuawa baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari moja kulipuka karibu la langu kuu la uwanja wa kimataifa a ndege katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa shambulio hilo lilikuwa limelenga msafara wa shirika la Umoja wa mataifa wa wakimbizi UNHCR.

Wengi wa waliouawa ni wapita njia na walinzi kadhaa wa Umoja wa Mataifa waliokuwa karibu na eneo la tukio hilo.

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu, limesema kuwa lilitekeleza shambulio hilo ambalo lilitokea katika eneo lenye ulinzi mkali mjini humo.

Majengo ya mengi ya ubalozi wa mataifa ya nchi za kigeni zimejengwa katika eneo hilo.

Wapiganaji hao wa Kiislamu walio na uhusiano na kundi la kigaidi la Aqaeda walitimuliwa kutoka Mogadishu miaka miwili iliyopita, lakini wamekuwa wakirejea mjini humo kufanya mashambulio ya mara kwa mara.

Magari ya Umoja wa Mataifa hayakuharibiwa vibaya wakati wa shambulio hilo.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wanajeshi wa Muungano wa Afrika wakishika doria mjini Mogadishu

Waandishi wa habaro nchini Somalia wanasema kuwa kumekuwa na mshambulio kadhaa mjini Mogadishu wiki iliyopita, huku wanamgambo hao wa Kisomali wakilenga kambi za jeshi la serikali.

Makombora yaliyorusha na wanamgambo hao kutoka umbali wa kilomita sita yamekuwa yakianguka katika uwanja mkuu wa ndege.

Wakaazi wa mji huo pia wameripoti kuongezeka kwa mashambulio ya mara kwa mara nyakati za usiku, hasa maeneo ya Kaskazini mwa mji huo.

Uwanja huo wa ndege ni kituo maalum cha wanajeshi wa kutunza amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia ambacho kinashirikiana na jeshi la serikali kutwaa uthibiti wa maeneo kadhaa ya nchi hiyo kutoka kwa wapiganaji wa Al-Shabaab.

Wapiganaji hao wa Al-Shabaab wamepoteza uthibiti wa miji muhimu, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, lakini bado inashikilia miji kadhaa Kusini mwa nchi hiyo.