Watoto kuamua kuhusu kifo Ubelgiji

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wabunge wa Ubelgiji wakijadili mswada huo

Wabunge Nchini Ubelgiji, wamepitisha sheria inayoruhusu mtoto kufanya maamuuzi kuhusu maswala ya kifo anapokuwa anaugua ugonjwa usio na tiba.

Hiyo imeifanya Ubelgiji kuwa taifa la kwanza duniani kupitisha sheria hiyo inayoruhusu mtu kuamua maisha yake kukatizwa kwa hiari yake mwenyewe au Euthanasia kwa lugha ya Kimombo.

Licha ya pingamizi kutoka kwa kanisa katoliki, idadi kubwa ya wabunge wa nchi hiyo waliunga mkono sheria hiyo, iliyoidhinishwa mwaka 2002, ambayo iliruhusu watu wazima kuchukua maamuzi kuhusu maisha yao wakiwa katika hali mahututi.

Sheria hiyo inasema kuwa ni sharti mtoto awe katika hali mbaya ya afya na katika hatari ya kufa kutokana na mahangaiko anayopata na pia katika hali nzuri kimawazo ili kuchukua uamuzi huo.

Lakini sasa sheria hiyo itatumika kwa watoto walio katika hatari ya kufa, iwapo watawasihi wazazi wao na madaktari kwamba wanataka kufa kama njia ya kuwaondolea mateso.