Kimbunga Uingereza chasababisha maafa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mafuriko nchini Uingereza

Maelfu ya nyumba nchini Uingereza hazina umeme na kumekuwa na matatizo makubwa katika usafiri wa umma baada ya upepo mkali kuipiga nchi hiyo Jumatano.

Wakati vyombo vya utabiri wa hali ya hewa vikielezea kuwepo upepo mkali Alhamisi, upepo mwingine mkali kutoka bahari ya Atlantiki utavuma kwa kasi ya karibu Kilomita 130 kwa saa kuanzia Ijumaa.

Tahadhari imekuwa ikitolewa kuhusu kuwepo mafuriko makubwa katika miji ya Berkshire, Surrey na Somerset - miji ambayo tayari imekumbwa na mafuriko makubwa.

Huduma za usafiri wa treni katika baadhi ya sehemu za jiji la London, zimesitishwa na barabara zimefungwa.

Jumatano mchana, mwanaume mmoja mwenye kukadiriwa umri wa miaka 70, aliuawa kwa umeme katika eneo la Bremhill, Wiltshire, baada ya mti kuangukia nyaya za umeme.