Je watoto waruhusiwe kifo cha huruma?

Haki miliki ya picha Science Photo Library
Image caption Bunge la waakilishi huenda likaidhinisha mswada huo

Bunge la Ubelgiji leo linatarajiwa kupigia kura mswada utakaowezesha watoto walio na ugonjwa usiotibika wakubaliwe kufa kifo cha huruma au 'Euthanasia'.

Inaarifiwa kuwa bunge la waakilishi huenda likaidhinisha mswada huo ambao utawaruhusu watoto waombe kusaidiwa kufa ikiwa wana ugonjwa usio na tiba, ikiwa wanahisi uchungu mwingi na pia kama hakuna matibabu ya kumponya.

Kwa sasa kwa raia wa Ubelgiji kuweza kupewa Euthanasia ni sharti awe ametimiza umri wa angalau miaka 18, kabla ya kupewa ruhusa ya kukubali asaidiwe kufa.

Chini ya sheria za sasa ombi la kufanyiwa hivyo kwa mtu asietimiza miaka 18 ni kwanza ombi lake likubaliwe na wazazi, madaktari pamoja na wataalamu wa Kisaikolojia.

Wale wanaopinga kubadilishwa kwa sheria hiyo wanahoji ikiwa mtoto anaweza kufanya uamuzi kama huo.

Hata hivyo daktari Yuta Van Der Verif, mtaalamu wa magonjwa ya watoto katika hospitali kuu mjini Brussels, anasema kuwa anaunga mkono mswada huo japo ni lazima mtoto asaidiwe katika uamuzi wake.

Kwa mswada huo kuwa sheria lazima utiwe saini na mfalme na kuifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza kuondoa kikwazo cha umri kwa watu wanaoweza kusaidiwa kufa.

Je nini maoni yako kuhusu hoja hii?

Tupe maoni yako kwenye ukurasa wetu wa facebook bbcswahili