Washambuliwa kwa kuvaa nguo fupi Kenya

Image caption Wasichana hao walikuwa wamevalia 'vinyasa' vilivyokuwa vimewabana mno

Kikundi cha wasichana kilinusurika kushambuliwa na wachuuzi mjini Kapsabet Magharibi mwa Kenya kwa kuvaa nguo zisizo za heshima.

Wanawake hao walishuka kutoka kwa basi la abiria wakiwa wamevalia 'Hot Pants' au vishoti vifupi sana na vilivyokuwa vinawabana katika soko moja mjini humo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa gazeti la Standard nchini Kenya Rael Jelimo mjini Eldoret, wanawake hao walikuwa wanauza vocha za moja ya kampuni kubwa za simu nchini humo.

Wanaume walipowaona wanawake hao waliwakimbiza na kuwazingira huku wakiwahoji kuhusu walivyovalia na hata kuwauliza ikiwa wanajua kama lazima wavalie nguo za heshima wakati wanapotoka nje za nyumba zao.

Jelimo ameambia BBC Swahili kuwa wachuuzi wanaume walioonekana kuchukizwa na ambavyo wanawake hao walikuwa wamevalia , waliwazingira nusura kuwavua nguo na kuwachapa.

Lakini waliokolewa na akina mama wenye saluni karibu na eneo hilo ambao baadaye waliwapa maleso kujifunika kabla ya kuokolewa na wenzao. waliwatetea kwa kusema kuwa hawatoki mjini humo na kwamba hawajui maadili ya watu wa mji huo.

Makampuni mengi ya simu na kampuni nyinginezo hutumia wasichana waliovalia vinguo vifupi na vya kubana kwa mauzo ya bidhaa zao. jambo hili bila shaka huwakera baadhi ya watu ila hawana namna ya kujieleza kuhusu mavazi kama hayo.

Swali, je ni sawa kuingilia mwanamke yeyote kuhusu alivyovalia na nguo alizovalia?