Kasisi afariki ghafla kwa 'rafiki' yake

Image caption Mwanamke amesema kuwa kasisi alikuwa nyumbani kwake kwa maombi

Kasisi mmoja mashuhuri wa kanisa moja nchini Kenya alizimia na kufariki dunia katika hali ya kutatanisha akiwa ndani ya nyumba ya mwanamke ambaye sie mke wake.

Tukio hili lilishuhudiwa katika mtaa wa Buruburu mjini Nairobi Kenya.

Mwili wa kasisi huyo kwa jina Geoffrey Maingi wa kanisa la Redeemed Gospel church mjini Nairobi, ulipatikana ndani ya chumba cha mwanamke huyo,baada ya kufarikini kutokana na sababu ambazo hazijulikani mnamo siku ya Jumanne.

Polisi walisema kuwa kasisi Maingi mwenye umri wa miaka 70, aliingia katika nyumba ya muumini mmoja wa kanisa lake kwa kile ambacho muumini huyo mwanamke alisema ilikuwa maombi maalum wakati alipofariki.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 40 ambaye alitalakiana na mumewe mwaka jana kutokana na ugomvui wa kinyumbani, aliambia polisi kuwa Maingi alikuwa amemtembelea kwa maombi kabla ya kuzirai na kufariki.

Kadhalika alisema kuwa kasisi huyo amekuwa akija nyumbani kwake kwa maombi,kwani mbali na kuwa kiongozi wake wa kanisa pia ni rafiki yake wa karibu.

Alihojiwa na kuachiliwa ingawa uchunguzi ungali unaendelea.

Kifo cha mzee huyo kilivutia hisia kutoka kwa majirani waliokuwa wanadai kuwa kasisi huyo alifariki kutokana na kutumia tembe za kuongeza nguvu mwili.