Kerry aikashifu vikali Boko Haram

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Shambulizi la Boko Haram

Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry ameshutumu mashambulizi ya hivi karibuni nchini Nigeria yaliyotekelezwa na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Katika taarifa yake Kerry alisema kuwa mashambulizi hayo ni maovu, mabaya na hayastahili kuwa yanaendelea duniani wakati huu.

Bwana Kerry ametoa taarifa yake wakati habari zinazotoka nchini Nigeria zikisema kumekuwa na mashambulizi mengine katika kijiji kimoja usiku wa kumkia leo ambapo hasara yake haijakadiriwa bado.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema kuwa Marekani itasaidia Serikali ya Nigeria kukabiliana na kundi hilo la Boko Haram ambalo limeorodheshwa na Marekani kama kundi la Kigaidi.

Mnamo Jumatano watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Boko Haram walishambulia mji wa Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo wa Bama katika Jimbo la Borno na kuwaua zaidi ya watu 100.

Jumapili iliyopita kundi hilohilo lilishambulia kijiji cha Igze na kuwaua watu wengine zaidi ya 100.

Bwana Kerry ameyasema haya wakati ambapo taarifa kutoka kijiji kilichoshambuliwa mnamo Jumapili iliyopita wanadaiwa kushambulia kijiji hicho tena usiku wa kumkia leo na kuteketeza nyumba, kuwapiga watu risasi na kulipua mabomu, kulingana na afisa mmoja kutoka eneo hilo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kerry akashifu Shambulizi la Boko Haram

Shambulizi la hivi majuzi zaidi lilifanywa saa saba usiku na mamia ya watu wamelazimika kutoroka makwao.

Mwenyekiti wa baraza la wilaya katika eneo la Madagali anasema kuwa hakuna chochote kilichopatikana kimesimama isipokuwa majivu.

Ingawa katika shambulio la kwanza la Februari 15 wazee na watoto walibakia katika nyumba lakini wakati huu wote walilazimika kutoroka kwa sababu ya kuchomewa makaazi na maghala ya vyakula.

Juma lililopita ilikishwa kuwa zaidi ya watu 10,000 walitoroka kijiji cha Izge na vitongoji vyake.

Wengi wao walitorokea miji ya karibu lakini sasa inadaiwa kwamba miji hiyo imefurika watu ambao wanaishi katika hali ya kusikitisha na mashirika ya kutoa misaada haijawafikia.

Kundi la Boko Haram limekuwa likishambulia maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria tangu mwaka 2009.

Kundi hilo, linasema linataka kuunda taifa linaloongozwa na Sheria za Kiislamu.

Serikali ya Nigeria imetangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Adamawa na yote tangu Mei mwaka uliopita.