Jeshi la Nigeria 'lipo thabiti'

Haki miliki ya picha nigeria villa
Image caption Rais Jonathan ameahidi ulinzi katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ghasia

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amesema anatarajia vita dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram, vitaendelea na ameahidi kutoa ulinzi kwa raia katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ghasia hizo.

Alikuwa akijibu shutuma za hivi karibuni, kuwa jeshi la nchini hiyo limeshindwa kuyashughulikia mashambulio ya Boko Haram na pia kutoimarika kwa hali ya ulinzi licha ya kutangazwa kwa hali ya hatari katika majimbo matatu ili kuzuia ghasia hizo.

Kiongozi huyo amesema ni jambo la kawaida kwa watu katika maeneo yaliyoathiriwa kaskazini mashariki mwa Nigeria, kuhisi kuwa serikali haijawapa ulinzi wanaostahili na wakati huo huo kutoa hakikisho kuwa hali hiyo itaimarishwa.

Uwezo wa Boko Haram

Lakini rais huyo alighadhabishwa na tangazo la hivi maajuzi la gavana wa jimbo la Borno, Kashim Shettima kuwa wapiganaji hao wa Boko Haram wana silaha zaidi kuliko jeshi la Serikali na kuwa wanalipwa zaidi ya wanajeshi wake.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais Jonathan ameitetea hadhi ya jeshi Nigeria

Rais Goodluck amesema ikiwa gavana huyo alihisi kuwa wanajeshi hawana maana yoyote, angeliwaondoa kutoka jimbo hilo kwa muda wa mwezi mmoja. Hali ambayo alisema itakuwa hata vigumu zaidi kwa gavana huyo kuishi katika eneo hilo.

Matamshi yake huenda yakaibua hasira miongoni mwa wakaazi wa jimbo la Borno ambao maisha yao yameharibiwa sana na ghasia. Watu wamelalamika kuwa kwa wakati mwingine mashambulio ya Boko Haram hudumu kwa saa kadhaa bila ya kuwepo kwa usaidizi wowote kutoka kwa jeshi la serikali.

Katika mahojiano na runinga ya taifa, rais Jonathan vile vile alitetea uamuzi wake wa kumfuta kazi Gavana wa benki kuu ya Nigeria Lamido Sanusi.

Amesema Sanusi alijiondoa ili kuruhusu uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya utumizi mbaya wa mamlaka na pia ufisadi.