Haki ya matibabu Uganda Licha ya sheria

Haki miliki ya picha
Image caption Haki ya Matibabu kwa wote Uganda

Waziri wa afya nchini Uganda, Daktari Ru-hakama Rugunda, amesema kuwa wapenzi wa jinsia moja hawatabaguliwa watakapokuwa wakihitaji huduma ya matibabu.

Hii ni licha ya kuidhinishwa kwa sheria mpya zinazopinga mapenzi ya jinsia moja Jumatatu wiki hii.

Mashirika ya kupambana na ukimwi yamesema sheria hiyo itakuwa na athari mbaya katika juhudi za kukabiliana na kuenea kwa virusi vya HIV.

Daktari Rugunda alisema kuwa wapenzi wa jinsia moja wanapaswa kuwa wazi kwa watabibu, hasa wakati wanapojadiliana maswala ya virusi vinavyosababisha ukimwi, HIV.

Huduma duni ya afya nchini Uganda hutegemea zaidi misaada kutoka wafadhili wa kimataifa.

Hadi kufikia sasa Marekani imesema kuwa inachunguza upya misaada kwa mipango kadhaa inayogharamia nchini humo.

Daktari Rugunda alisema kuwa ana imani kwamba Marekani haitapunguza misaada yake ya kifedha lakini akasisitiza kuwa ikichukua hatua hiyo Uganda ingali itaendelea na shughuli zake kama kawaida.