26 wahukumiwa adhabu ya kifo Misri

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jeshi la Misri

Mahakama moja nchini Misri imewahukumu watu 26 adhabu ya kifo kwa kuanzisha "kikundi cha ugaidi" kwa lengo la kushambulia meli zinazotumia mfereji wa Suez.

Majaji waliosikiliza kesi hiyo wamesema watu hao pia walituhumiwa kutengeneza makombora na vilipuzi.

Washitakiwa walihukumiwa bila ya wao kuwepo mahakamani.

Adhabu hiyo imetolewa siku moja baada ya waziri mkuu mpya mteule wa Misri, Ibrahim Mehleb, kuapa "kutokomeza ugaidi katika pembe zote za nchi hiyo".

Bwana Mehleb amepewa madaraka ya kuunda serikali mpya kufuatia kujiuzulu kusikotarajiwa kwa aliyekuwa waziri mkuu wa muda Hazem Beblawi na baraza lake la mawaziri, Jumatatu.

Bwana Beblawi aliteuliwa Julai 2013 baada ya jeshi kumng'oa madarakani Rais Mohammed Morsi kutokana na maandamano makubwa.

Tangu wakati huo, zaidi ya watu 1,000 wameuawa na maelfu ya wengine kuwekwa kizuizini kufuatia msako uliofanywa na majeshi ya usalama dhidi ya kikundi cha Muslim Brotherhood, vuguvugu la Kiislam ambalo Bwana Morsi ni mwanachama wake.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ibrahim Mehleb,waziri mkuu mpya mteule wa Misri

Wakati huo huo wanamgambo walioko katika rasi ya Sinai wamekuwa wakiendesha mashambulio dhidi ya serikali, polisi na majeshi.

Katika hukumu ya Jumatano, mahakama ilisema watuhumiwa hao wameathiri "umoja wa kitaifa", kwa kuchochea ghasia dhidi ya jeshi, polisi na Wakristo.

Hukumu ya kesi hiyo itapelekwa kwa kiongozi wa juu wa dini ya Kiislam nchini Misri ambaye atathibitisha hukumu hiyo.

Hukumu ya mwisho inatarajiwa kutolewa tarehe 19 Marchi 2014.

Hakuna taarifa zaidi zilizopatikana kuhusu kundi hili linaloshitakiwa.

Na katika hatua nyingine, Bwana Mehleb ameanza kuteua mawaziri kadhaa katika serikali yake mpya.

Waziri mkuu mpya mteule alikuwa afisa mwandamizi katika chama tawala cha zamani cha Bwana Hosni Mubarak, na aliteuliwa kuwa mjumbe wa baraza la juu la bunge la Misri, Shura ambalo lilifutiliwa mbali mwaka 2010.