Wagonjwa wanalengwa Sudan kusini

Image caption MSF linasema wagonjwa wanauawa wakitibiwa vitandani

Shirika la madakatari wasio na mipaka MSF limeonya kwamba kazi zake zinasambaratishwa kutokana na mashambulio mabaya dhidi ya vituo vya afya ambapo wagonjwa na wahudumu wanalengwa.

Katika ripoti mpya ya shirika hilo, MSF inasema maelfu ya watu wananyimwa huduma ya kuyaokoa maisha yao.

Umoja wa mataifa unasema mapigano kati ya serikali na waasi tangu kati kati mwa mwezi Desemba yamesababisha watu 860,000 kupoteza makaazi yao.

Pande hizo mbili zimelaumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yalio tiwa saini mwezi Januari.

Haki miliki ya picha Liang Zi
Image caption MSF ina wafanyakazi 333 wa kimataifa Sudan kusini

Ripoti hiyo inasema, "wakati miji ya Sudan kusini inakabiliwa na mashambulio mabaya, huduma ya afya pia imelengwa, na wagonjwa wanapigwa risasi wakiwa vitandani, vyumba vya wagonjwa vinachomwa, vifaa vya afya vinaibiwa, na katika tukio moja, hospitali nzima iliharibiwa".

Mashambulio ya hivi karibuni

Ripoti hiyo inataja mashambulio mabaya ya hivi karibuni yakiwemo:

- Wagonjwa kuuawa wakihudumiwa katika mji wa Malakal katika jimbo la Upper Nile.

- Kuvamiwa, kuibiwa na kuchomwa kwa hospitali huko Leer, katika jimbo la Unity.

- Sehemu iliyoko MSF mjini Bentiu, ilichomwa wakati wa mapigano makali.

- Mnamo Februari 22, MSF iligundua miili ipatayo 14 katika sehemu ya hospitali ya mafunzo huko Malakal, iliyotapakaa miongoni mwa wagonjwa kati ya 50 na 75 waliodhohofika au wakongwe walioshindwa kukimbilia usalama wao.

Ushahidi uliopo

"Wagonjwa kadhaa walionekana kupigwa risasi kichwani wakiwa wamelala vitandani mwao" ilisema ripoti hiyo.

"Vyumba vingi vya wagonjwa kikiwemo cha matibabu kwa watoto walio na matatizo ya lishe bora, vilichomwa, na maeneo mengi ya hospitali hiyo yalichomwa."

Image caption Pande zote zinalaumiana kwa kutositisha mapigano.

Malakal, mji ulio na soko, ulio na kiingilio kikuu kwa ardhi ya uchimbaji mafuta katika jimbo la Upper Nile, umegubikwa kwa mapigano na umedhibitiwa na pande zote mara kwa mara.

Mratibu wa huduma za dharura wa MSF katika eneo hilo, Carlos Francisco anasema, " hana maneno ya kuelezea uovu unaofanyika Malakal, uliosababisha kusalia kwa mji uliovamiwa, na watu walioathirika pakubwa na hofu walio nayo".

Kilichoanza kama mzozo wa kisiasa kati ya rais Salva Kiir na aliyekuwa naibu wake Riek Machar, kiligeuka na kuwa mzozo mkubwa huku sehemu ya mapigano hayo yakiwa ya kikabila.

MSF ina wafanyakazi 333 wa kimataifa wanaofanya kazi katika miradi yake kwa ushirikiano wa maafisa 3,330 kutoka Sudan kusini.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii