Viwanja vya ndege vyadhibitiwa Crimea

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu wenye silaha wakilinda doria uwanja wa ndege Simferopol, Crimea, Ukraine

Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine amesema majeshi ya Urusi yamekuwa yakiweka vizuizi katika uwanja wa ndege wa Sevastopol uliopo katika jimbo la Crimea.

Waziri huyo wa Ukraine, Arsen Avakov ameita uwepo wa majeshi ya Urusi katika jimbo hilo kuwa "uvamizi wa kijeshi".

Watu hao wenye silaha pia wameutwaa uwanja mwingine mkubwa wa ndege wa Simferopol, uliopo pia Crimea Ijumaa asubuhi.

Uhusiano kati ya Urusi na Ukraine umeyumba tangu kuondolewa madarakani kwa Rais wa Ukraine, Viktor Yanokovych, ambaye kwa sasa yuko nchini Urusi.

Uhasama huu umedhihirika zaidi katika jimbo la Crimea, nchini Ukraine, ambalo wakaazi wake wengi ni Warusi.

Siku ya Alhamisi, watu wenye silaha wenye mwelekeo wa Urusi, walivamia ofisi za bunge la Simferopol, na kuliondoa baraza la sasa la mawaziri na kumchagua waziri mkuu mpya.

Bado haijafahamika watu hawa wenye silaha katika mji wa Simferopol waliowasili katika uwanja wa ndege mapema ni kina nani.

Licha ya kuwepo kwao, inasemekana shughuli zinaendelea kama kawaida katika uwanja wa ndege wa Simferopol.

Watu walioshuhudia tukio hilo wameliambia shirika la habari la Ukraine, Interfax, kuwa watu wapatao 50 waliwasili katika uwanja wa ndege wa Simferopol wakiwa wamebeba bendera za jeshi la wanawamaji la Urusi.